Mafanikio si bahati. Mara nyingi ni matokeo ya namna unavyofikiri, unavyofanya maamuzi, unavyokabiliana na makosa na unavyojifunza kutokana na maisha. Kila siku tunafanya maamuzi mengi. Baadhi yanaonekana madogo sana, kama namna tunavyotumia muda, tunavyojibu changamoto au tunavyotumia pesa. Mengine ni makubwa zaidi, kama kazi gani tufanye, biashara gani tuanzishe, nani tushirikiane naye, au ni hatari gani tuchukue. Ingawa hatuwezi kujua kila kitu kitakachotokea, tunaweza kujifunza namna bora ya kufikiri na kukabiliana na kile kinachotokea.
Hapo ndipo umuhimu wa kuwa na kanuni za maisha unapoanzia. Kanuni ni njia za kufikiri na kutenda zinazokusaidia kufanya maamuzi mazuri unapokutana na hali zinazojirudia. Badala ya kuishi kwa kubahatisha, unaweza kujenga mfumo unaokusaidia kujifunza, kubadilika na kuendelea kukua. Kadiri unavyokuwa na kanuni zilizo wazi, ndivyo inavyokuwa rahisi kufanya maamuzi yenye mantiki hata unapokuwa chini ya presha, unapokuwa umeumia au unapokabiliwa na hali usiyoitarajia.
Jifunze Kufikiri kwa Kichwa Chako
Moja ya uwezo mkubwa unaoweza kujenga katika maisha ni uwezo wa kufikiri kwa kujitegemea. Maisha yetu yanaathiriwa sana na mawazo ya wengine. Familia inaweza kukuambia mafanikio yanapaswa kuonekana kwa namna fulani. Jamii inaweza kukuambia kazi nzuri ni ipi. Marafiki wanaweza kukuonyesha maisha unayopaswa kutamani, huku mitandao ya kijamii ikikufanya uamini kwamba mafanikio yanamaanisha pesa nyingi, magari, nyumba, umaarufu au followers wengi.
Lakini mwisho wa siku, ni wewe utakayeishi na matokeo ya maamuzi yako. Kwa hiyo badala ya kujiuliza kila wakati watu wengine wanafanya nini, jifunze kujiuliza, “Ni nini kweli, na ni nini kinachofaa kwa maisha ninayotaka kujenga?” Usifuate mkumbo bila kufikiri. Jenga uwezo wa kuchunguza, kuhoji na kufanya maamuzi yanayotokana na maadili yako, malengo yako na uhalisia wa mazingira yako.
Kufikiri kwa kichwa chako haimaanishi kupuuza ushauri wa watu wengine. Maana yake ni kutokubali jambo kwa sababu tu limesemwa na wengi. Sikiliza, chunguza, linganisha, tafakari, halafu fanya uamuzi unaoona unaendana zaidi na ukweli uliopo.
Kubali Kwamba Hujui Kila Kitu
Watu wengi hudhani kuonekana unajua kila kitu ni ishara ya akili. Ukweli ni kwamba mtu mwenye hekima zaidi mara nyingi ni yule anayeweza kukubali kwamba huenda kuna jambo hajaliona au hajalielewa vizuri. Kukubali kwamba hujui si udhaifu. Ni mwanzo wa kujifunza.
Tatizo linaanza pale tunapokuwa na hamu kubwa zaidi ya kuonekana tuko sahihi kuliko kutafuta kilicho sahihi. Tunaweza kushikilia wazo hata pale ushahidi unaonyesha vinginevyo kwa sababu tu hatutaki kukubali kwamba tulikosea. Tunaweza kukataa ushauri mzuri kwa sababu umetoka kwa mtu ambaye hatukutegemea kuwa na jibu bora kuliko letu.
Badala ya kuwa na uhakika kupita kiasi kwamba mpango wako lazima ufanye kazi, jifunze kujiuliza ni nini kinaweza kuufanya ushindwe. Badala ya kumkataa mtu anayepingana nawe, jiulize kama kuna kitu anachokiona ambacho wewe hujakiona. Kadiri unavyokuwa tayari kukubali uwezekano wa kukosea, ndivyo unavyojenga uwezo mkubwa zaidi wa kufanya maamuzi bora.
Kubali Uhalisia Ulivyo
Ndoto ni muhimu, lakini ndoto bila uhalisia zinaweza kubaki kuwa matamanio. Unaweza kutamani biashara yako ikue, lakini kama mauzo ni madogo, lazima ukubali ukweli huo kwanza. Unaweza kutaka kuwa na fedha nyingi, lakini kama matumizi yako hayana nidhamu, lazima ulione hilo. Unaweza kutaka afya nzuri, lakini kama tabia zako haziungi mkono afya hiyo, lazima ukubali hali ilivyo.
Huwezi kubadilisha kitu ambacho hukubali kwamba kina tatizo. Ndoto kubwa zinapaswa kwenda sambamba na uhalisia na dhamira ya kuchukua hatua. Ndoto inakuonyesha unapotaka kwenda, uhalisia unakuonyesha ulipo sasa, na dhamira pamoja na utekelezaji vinakusaidia kuvuka pengo lililopo kati ya sehemu hizo mbili.
Ukweli wakati mwingine unaweza kuuma, lakini mara nyingi ndiyo taarifa muhimu zaidi unayohitaji ili kubadilika. Kukataa hali halisi hakufanyi tatizo liondoke. Kunalifanya tu liendelee kukua huku wewe ukiendelea kuishi katika picha ambayo si halisi.
Tumia Maumivu Kama Darasa
Kushindwa kunauma. Kupoteza pesa kunauma. Kukataliwa kunauma. Kufanya uamuzi mbaya kunauma. Kuamini jambo kwa nguvu halafu kugundua kwamba ulikosea kunaweza kuumiza sana. Lakini maumivu pekee hayakufanyi kuwa bora. Kinachokufanya kuwa bora ni kile unachofanya baada ya maumivu hayo.
Kanuni muhimu hapa ni kwamba maumivu yakifuatwa na tafakari yanaweza kuzaa maendeleo. Ukiumia bila kutafakari, unaweza kuishia na hasira, hofu, lawama au kukata tamaa. Lakini ukisimama na kuchunguza kilichotokea, kwa nini kilitokea, mchango wako ulikuwa upi na ungeweza kufanya nini tofauti, maumivu yanaanza kubadilika kuwa somo.
Badala ya kuuliza kila wakati, “Kwa nini hili limenitokea?” unaweza kuanza kuuliza, “Hili linanifundisha nini?” Swali hili linaweza kubadili namna unavyotazama changamoto. Kosa linapoacha kuwa hasara tu na kuanza kuwa chanzo cha maarifa, linakuwa sehemu ya ukuaji wako.
Mfumo wa Hatua Tano wa Kufikia Malengo
Maendeleo mengi yanaweza kueleweka kupitia mfumo rahisi wa hatua tano. Hatua ya kwanza ni kujua unachotaka. Huwezi kufika mahali usipopajua. Unahitaji kuelewa ni maisha ya aina gani unayotaka, unataka kufanikisha nini, ni mambo gani muhimu zaidi kwako na ni gharama gani uko tayari kulipa ili kufikia malengo yako. Malengo yako hayapaswi kujengwa kwa sababu tu yanaonekana mazuri mbele ya watu. Yanapaswa kuendana na maisha unayotaka kweli.
Hatua ya pili ni kutambua matatizo yanayokuzuia. Kati yako na kila lengo kuna vikwazo. Kama biashara yako haina wateja wa kutosha, hilo ni tatizo. Kama unataka kujifunza lakini huwezi kukaa muda mfupi bila kushika simu, hilo ni tatizo. Kama unataka kuweka akiba lakini kila mwezi unatumia kila unachopata, hilo ni tatizo. Tatizo usilolikubali huwezi kulitatua.
Hatua ya tatu ni kutafuta chanzo halisi cha tatizo. Watu wengi hukimbilia suluhisho kabla hawajaelewa tatizo. Mauzo yakishuka, mtu anaweza kusema aongeze matangazo. Lakini huenda matangazo si tatizo. Huenda bidhaa haijaelezwa vizuri, bei hailingani na thamani, wateja wanaolengwa si sahihi, au hakuna mfumo mzuri wa kuwafuatilia watu walioonyesha nia ya kununua. Ni muhimu kutenganisha dalili na chanzo.
Hatua ya nne ni kutengeneza mpango. Baada ya kuelewa chanzo, amua ni nini unahitaji kufanya, ni nini unapaswa kuacha, ni nini unapaswa kuanza, nani anaweza kukusaidia na utapimaje matokeo. Mpango mzuri unabadilisha tatizo kutoka kitu kinachokutisha na kuwa jambo lenye hatua maalumu za kulishughulikia.
Hatua ya tano ni utekelezaji. Hii ndiyo sehemu ambayo watu wengi hukwama. Unaweza kusoma vitabu vingi, kuhudhuria semina, kuandika malengo na kutengeneza mipango mizuri sana, lakini bila utekelezaji hakuna kinachobadilika. Mfumo huo kwa ufupi ni: lengo, tatizo, chanzo, mpango na utekelezaji. Baada ya hapo unapima matokeo, unajifunza, unarekebisha na kuanza mzunguko mwingine.
Kushindwa Si Mwisho, Ni Taarifa
Kushindwa hakuthibitishi kwamba huwezi. Mara nyingi kunakupa taarifa kwamba kuna jambo bado hulijui, hulielewi au hujalifanya vizuri. Badala ya kusema, “Mimi ni mshindwa,” unaweza kusema, “Njia niliyotumia haikufanya kazi. Kwa nini?”
Hii ni tofauti kubwa sana. Mtu anayejifunza hahusishi kosa moja na thamani yake kama binadamu. Analichunguza kosa, anatafuta sababu, anatengeneza kanuni na anajaribu tena akiwa na maarifa zaidi. Kushindwa kunapaswa kukufanya mnyenyekevu, si mnyonge. Unyenyekevu unasema, “Nilikosea, lakini ninaweza kujifunza.” Unyonge unasema, “Nilikosea, kwa hiyo mimi siwezi.”
Watu wengi ambao baadaye wamefanikiwa walipitia nyakati ambazo wangeweza kuamini kila kitu kimekwisha. Kilichowatofautisha ni uwezo wa kutafsiri kushindwa kwao kama sehemu ya mchakato wa kujifunza badala ya hukumu ya mwisho juu ya uwezo wao.
Jihadhari na Ego Yako
Mmoja wa maadui wakubwa wa ukuaji wako anaweza kuwa ego yako mwenyewe. Ego inataka uthibitishwe, isifiwe na isikosolewe. Haitaki ukiri kwamba umefanya kosa. Haitaki mwingine aonekane anajua zaidi yako. Lakini unapolinda taswira yako kuliko unavyolinda ukweli, unapunguza uwezo wako wa kujifunza.
Jiulize kama unataka kuwa sahihi au unataka kujua kilicho sahihi. Mambo hayo mawili hayafanani. Kama lengo lako ni kuthibitisha kwamba uko sahihi, utaona ukosoaji kama shambulio. Kama lengo lako ni kupata ukweli, utaona ukosoaji wenye msingi kama taarifa muhimu.
Mtu anaweza kukuambia kwamba mpango wako una tatizo, bidhaa yako haieleweki au una tabia inayokuzuia kukua. Kauli hiyo inaweza kuumiza ego yako, lakini ikiwa ina ukweli ndani yake, inaweza kuwa moja ya taarifa muhimu zaidi utakazopokea.
Kubali Kwamba Una Blind Spots
Hakuna mtu anayeona picha yote. Kila mmoja wetu ana maeneo anayoyaona vizuri na maeneo ambayo hayako ndani ya uwezo wake wa asili. Unaweza kuwa mzuri katika kuona picha kubwa lakini dhaifu katika maelezo. Unaweza kuwa mbunifu sana lakini dhaifu katika utekelezaji. Unaweza kuwa jasiri lakini ukachukua hatari nyingi. Unaweza kuwa mwangalifu sana kiasi cha kupoteza fursa.
Hizi ni blind spots, yaani maeneo ambayo uwezo wako wa kuona au kuelewa ni mdogo bila wewe kujua. Tatizo si kuwa nazo kwa sababu kila mtu anazo. Tatizo ni kufikiri kwamba huna.
Mara nyingi nguvu yetu kubwa inaweza pia kuwa chanzo cha udhaifu wetu. Mtu mwenye kujiamini sana anaweza kuwa jasiri, lakini pia anaweza kuwa mgumu kusikiliza. Mtu mwenye tahadhari anaweza kufanya maamuzi salama, lakini tahadhari hiyo hiyo inaweza kumzuia kuchukua fursa. Kujitambua kunahitaji kuona pande zote mbili.
Jizungushe na Watu Wanaoweza Kuona Usichokiona
Usitafute watu watakaosema “ndiyo” kwa kila unachosema. Tafuta watu wenye uwezo wa kusema, “Sikubaliani nawe, na hii ndiyo sababu.” Kuna tofauti kubwa kati ya mabishano na majadiliano yenye tija. Katika mabishano, kila mtu anataka kushinda. Katika majadiliano yenye tija, kila mtu anataka kugundua ukweli.
Kama wewe ni mbunifu, huenda ukahitaji mtu anayependa mifumo. Kama wewe ni mtu wa kasi, huenda ukahitaji mtu wa tahadhari. Kama wewe ni mtu wa maono, huenda ukahitaji mtu wa maelezo. Kama wewe ni mchambuzi sana, huenda ukahitaji mtu mwenye uwezo mkubwa wa kutekeleza.
Huhitaji kuwa bora katika kila kitu. Unahitaji kujua nguvu zako, udhaifu wako na watu wanaoweza kukamilisha uwezo wako. Mara nyingi mafanikio makubwa hayaji kwa sababu mtu mmoja anajua kila kitu, bali kwa sababu anajua namna ya kufanya kazi na watu wanaoona mambo ambayo yeye hawezi kuona.
Si Kila Maoni Lina Uzito Sawa
Kuwasikiliza watu hakumaanishi kufuata kila ushauri unaopewa. Maoni yote hayana uzito sawa. Ni muhimu kuangalia uzoefu wa mtu, rekodi yake, uwezo wake wa kueleza sababu za anachoamini na kama amewahi kufanikiwa katika eneo analokupa ushauri.
Usichague ushauri kwa sababu tu unapenda kuusikia. Mara nyingi ushauri unaotufurahisha zaidi ndiyo tunaoutaka hata kama hauna ushahidi wa kutosha. Jifunze kutafuta watu wenye uwezo wa kufikiri vizuri, uzoefu unaohusiana na tatizo lako na utayari wa kukuambia ukweli hata kama si rahisi kuusikia.
Jifunze Kusawazisha Hatari na Faida
Maisha bila hatari yanaweza kuonekana salama, lakini pia yanaweza kukunyima fursa nyingi. Biashara ina hatari. Uwekezaji una hatari. Kubadilisha kazi kuna hatari. Kufuata ndoto kuna hatari. Hata kutofanya chochote kuna hatari yake kwa sababu unaweza kupoteza muda na fursa.
Lengo si kuondoa hatari zote. Lengo ni kuelewa na kusimamia hatari. Kabla ya kufanya uamuzi mkubwa, jiulize nini kitatokea ukikosea, unaweza kupoteza kiasi gani, unaweza kurudi tena, umeweka kila kitu kwenye uamuzi mmoja au una njia ya kujilinda.
Hatari nzuri ni ile ambayo inaweza kukupa fursa ya kukua bila kukuweka katika mazingira ambayo kosa moja linaweza kukuangamiza kabisa. Ujasiri haupaswi kuwa uzembe. Mtu mwenye hekima anajifunza kuwa jasiri huku akiendelea kuheshimu hatari.
Mafanikio ya Kweli Ni Ukuaji
Mara nyingi tunafikiri mafanikio ni kufikia lengo fulani. Tunajiambia kwamba tukipata kiasi fulani cha pesa, cheo fulani, biashara kubwa au mafanikio fulani tutakuwa tumefika. Lakini baada ya kufikia malengo mengi, mara nyingi tunaanza kutafuta mengine.
Huenda sababu ni kwamba zawadi kubwa si lengo lenyewe. Zawadi kubwa ni mtu tunayekuwa wakati wa kulifuatilia. Changamoto zinatufundisha, makosa yanatukomaza, majukumu yanatujenga na matatizo yanatulazimisha kuongeza uwezo wetu.
Kwa hiyo mafanikio si maisha yasiyo na matatizo. Mafanikio ni kuwa mtu mwenye uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na matatizo makubwa zaidi. Kadiri unavyokua, changamoto zako zinaweza pia kukua, lakini uwezo wako wa kuzishughulikia unakuwa mkubwa zaidi.
Geuza Maisha Yako Kuwa Mfumo wa Kujiboresha
Njia nzuri ya kuishi ni kugeuza maisha yako kuwa mzunguko wa kujifunza. Jaribu kitu, angalia matokeo, tafakari, jifunze, rekebisha na ujaribu tena. Ukifanya hivyo mara kwa mara, makosa yako yataanza kutoa kanuni ambazo unaweza kutumia katika maamuzi yajayo.
Kwa mfano, unaweza kujifunza kupitia uzoefu wako kwamba hutafanya tena uamuzi mkubwa wa kifedha kwa hisia. Unaweza kujifunza kutopanua biashara kabla mfumo wa sasa haujathibitishwa. Unaweza kujifunza kwamba kadiri uamuzi unavyoweza kukugharimu zaidi, ndivyo unavyopaswa kutafuta taarifa na mitazamo zaidi kabla ya kuufanya.
Baada ya muda, utaanza kujenga mfumo wako binafsi wa kuendesha maisha. Hutakuwa tena unatatua kila tatizo kana kwamba ni mara ya kwanza kuliona. Utakuwa unaingia katika changamoto ukiwa na kanuni, uzoefu na mfumo wa kufikiri ulioujenga kutokana na maisha yako mwenyewe.
Hatua ya Kuchukua Leo
Usimalize kusoma makala hii halafu urudi katika maisha yako kama kawaida. Chukua muda na ujiulize lengo kubwa zaidi unalotaka kufikia kwa sasa ni lipi. Jiulize ni matatizo gani yanayokuzuia, chanzo chake ni nini na ni hatua gani unapaswa kuchukua. Kumbuka pia kosa kubwa ulilofanya ambalo bado hujaligeuza kuwa somo. Fikiria udhaifu ambao huenda hauuoni vizuri na mtu ambaye anaweza kukusaidia kuona mambo kwa mtazamo tofauti.
Kisha tengeneza kanuni moja mpya ambayo utaanza kuishi nayo kuanzia leo. Inaweza kuwa kanuni kuhusu fedha, biashara, muda, mahusiano, afya au maamuzi. Jambo muhimu ni kuhakikisha kwamba uzoefu wako wa jana unakusaidia kufanya maamuzi bora leo.
Hitimisho
Maisha makubwa hayajengwi kwa kutokosea. Yanajengwa kwa kujifunza vizuri kila unapokosea. Fikiri kwa kichwa chako, kubali uhalisia, usikimbie matatizo, tafuta chanzo chake, tengeneza mpango na utekeleze. Ukikosea, tafakari. Ukiumia, jifunze. Ukifanikiwa, endelea kuwa mnyenyekevu. Unapokosa kuona njia, tumia macho ya watu wanaoweza kuona kile ambacho wewe huoni.
Kumbuka kwamba maumivu yakifuatwa na tafakari yanaweza kuzaa maendeleo. Kumbuka pia kwamba safari ya kufikia lengo inaanza kwa kujua unachotaka, kutambua matatizo yanayokuzuia, kutafuta chanzo chake, kutengeneza mpango na kuutekeleza. Ukirudia mzunguko huo mara kwa mara, hautakuwa tu unafikia malengo. Utakuwa unajenga toleo bora zaidi la wewe mwenyewe.
Mwishowe, mafanikio ya kweli si tu kufika unakotaka kwenda. Ni kuwa mtu bora zaidi katika safari ya kufika huko, kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto kubwa zaidi na kutumia kila ushindi, kosa na maumivu kama sehemu ya ukuaji wako.
Je, ni kanuni gani moja ambayo umejifunza kupitia kosa au changamoto kubwa katika maisha yako? Shiriki kwenye sehemu ya maoni. Somo lako linaweza kumsaidia mtu mwingine kufanya uamuzi bora zaidi katika maisha yake.
